EAC integration process on course

Spika EALA: Jumuiya    

EAC inakwenda vizuri

 

*Changamoto hazikoskeni, kila linalojitokeza ni funzo kwetu

* Tutaipeleka haraka miswada ya kutupeleka Umoja wa Sarafu

*Hatua za kujenga Reli ya

Kisasa ni muhimu kwa ujiranimwema

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inayoundwa na nchi sita, inaendelea na mchakato wake wa kuelekea kwenye shirikisho la kisiasa. Pamoja na mambo mengine, Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EALA), MARTIN NGOGA, anaelezea mwelekeo wa jumuiya hiyo kama alivyofanya mahojiano maalum na mwandishi wetu, NICODEMUS IKONKO.

 

SWALI: Ni miezi ipatayo minne sasa tangu uchaguliwe kuwa Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EALA). Unadhani Jumuiya hiyo iko katika mwelekeo sahihi wa kufikia malengo yake ya mtangamano wake?

 

JIBU: Asante sana. Mimi nafikiri wazo zima la kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, malengo na falsafa yake ni zuri sana na si jipya kwa sababu historia inajulikana. Juhudi za kwanza za kuwa na jumuiya za kuweka nchi zetu pamoja zilianza mara baada ya uhuru na baadaye kukawa na matatizo. Juhudi zikafanyika kuianzisha upya.

Kwa hiyo lengo ni zuri. Kuhusu mwelekeo na tunavyoendelea mpaka sasa hivi mimi nafikiri tunaendelea vizuri. Kwa sababu hatua tuliyofikia katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa upya kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni hatua kubwa. Lazima tuzingatie kwamba mradi wa jumuiya si mradi mdogo. Unajumuisha nchi sita huku kila moja ikiwa nchi huru, yenye mamlaka, malengo na vipaumbele vyake. Jumuiya ni juhudi za kuweka vipaumbele vyetu pamoja.

Mimi nafikiri tunaendele vizuri katika maeneo ambayo tayari tumeshakubaliana. Itifaki ambazo zimesainiwa na zimeendelea kutekelezwa zinakwenda vizuri. Kuna matatizo madogo madogo ambayo lazima yatarajiwe kuwa yatakuwepo na kila tatizo linalojitokeza ni funzo kwetu.

Zipo changamoto ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa hatua nne tulizojiwekea kufikia hatua ya mwisho ya mtangamano wetu ambao ni Shirikisho la Kisiasa bado ziko nyuma kidogo. Lakini tunafanya juhudi za kwenda haraka zaidi.

Nafikiri mmesikia tukitangaza kwamba kuna baadhi ya miswada ya sheria ambayo tutajaribu kuipeleka haraka sana ambayo inagusia uanzishwashwaji wa baadhi ya taasisi zitakazotuwezesha kuelekea Umoja wa Sarafu.

Katika ratiba tuliyokuwa tumejiwekea tupo nyuma kwa miaka miwili sasa. Lakini hilo si tatizo kubwa, suala la msingi ni kwamba bado tuna utashi na juhudi zinafanyika tuendelee kusonga mbele tufikie malengo tuliyojiwekea kwenye jumuiya.

SWALI: Mheshimiwa, wewe ni Spika wa tano wa EALA, una mikakati gani katika kipindi chako cha uongozi wa jumuiya kupitia nafasi hiyo uliyonayo?

JIBU

Mimi ninavyoielewa kazi ya Spika nafikiri si kazi ambayo inakuja na mikakati binafsi ya kiongozi anayekuwepo kwa sababu kazi ya spika ni kazi ambayo imeandaliwa kisheria, kuna utaratibu wa sheria wa Bunge.

Je, Bunge linatakiwa lifanye nini kwa mujibu wa mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya. Spika hatarajiwi kuwa mbunifu kujiongezea yale ambayo sheria haijampatia.

Jukumu kubwa la Spika ni kuhakikisha kwamba Bunge linafikia malengo yake ambayo yameandaliwa kisheria na tunafikiri tutafanya juhudi za pamoja si spika tu mimi mwenyewe bali na wabunge wenzangu kutoka nchi zote wanachama wa jumuiya tutajitahidi na tumeanza tayari. Majukumu ya bunge la Afrika mashariki yapo ya aina tatu. Moja ni jukumu la kutunga sheria, ambazo zinawezesha utekelezaji wa maeneo mbalimbali ya itifaki ambayo tayari tumeshakubaliana kwa ushirikiano wetu.

Tunayo pia kazi ya kuwakilisha wananchi wetu, kama bunge lolote lile, kuwasikiliza na kujua matunda ya ushirikiano wetu yanawafikia na kama yanawafikia wanafaidika vipi, kama kuna matatizo ni yapi na yako wapi ili tutoe ushauri pale matatizo yanaonekana ili yarekebishwe.

Tunalo jukumu pia la kuangalia utendaji wa taasisi zingine, sekretarierti na taasisi zote za jumuiya kuhusu namna wanavyotumia rasilimali ambazo wamepewa kutekeleze majukumu yao. Kwa mfano kuwataka mawaziri walete ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Fedha ili tuweze kuijadili Bungeni.

Kwa hiyo majukumu yetu yapo katika sheria na tunafahamu na tunajua mipaka yake. Ahadi ambayo niliwapa wenzangu na nawapa wananchi wote na wakazi wa jumuiya hii ni kwamba bunge la nne la Jumuiya ya Afrika Mashariki litajitahidi kutimiza malengo yake na tunaamini kwamba mchango wetu ni mkubwa sana katika kuharakisha utendaji wa taasisi zingine zote katika maeneo ya ushirikiano ambayo tayari tumeshakubaliana.

SWALI: Tanzania na Rwanda zinatekeleza uchumi wa viwanda ambao unaalika wawekezaji kutoka ndani na nje kujenga viwanda mbalimbali vikiwemo vya nguo. Katika utekelezaji zimekuwepo baadhi za nchi za viwanda ulimwenguni ambazo hazifurahii hatua hiyo kutokana na ukweli kwamba soko la nguo za mitumba kutoka nchi hizo linatishiwa kutoweka. Unasemaje kuhusu dhana hii ambayo inanekana kuwa kikwazo kwa sera ya viwanda Afrika Mashariki?

JIBU: Nafikiri kuna makubaliano yalifikiwa kwamba ili tuweze kuendeleza viwanda vyetu vya ndani lazima tuzuie hasa matumizi ya nguo za mitumba kuingizwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sasa baada ya huo uamuzi kulitokea mrejesho kutoka baadhi yetu tuliokuwa hatujajiandaa kuzipokea na ikasababisha utekelezaji wa huo uamuzi utetereke kidogo.

Zipo baadhi ya nchi wanachama ambazo bado wanaendelea kutekeleza uamuzi huo kuhusu nguo ziliozitumika kutoka nje ziingizwe kwa kutozwa kodi kubwa sana ambayo ni njia mojawapo ya kuzipunguza na zinaamini kwamba kwa kufanya hivyo watachochea kukua kwa viwanda vya ndani lakini pia zipo nchi nyingine ambazo zimeamua kujipa muda wa kuliangalia suala hilo upya, si kwamba wameachana kabisa na uamuzi wenyewe, wanafikiria wanaweza kutekeleza kwa awamu.

Changamoto kama hizo zilitarajiwa. Mnapokuwa nchi sita na mmechukua uamuzi fulani ni wazi katika hatua ya awali wataangalia mambo mbalimbali ambayo kuna wakati mnaweza kutofautiana. Lakini wazo zima ni kwamba ili tukuze viwanda vya ndani lazima tupunguze matumizi ya nguo kutoka nje hasa ambazo zimetumika tayari.

Mimi sidhani kama kuna nchi yoyote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki imechana nayo ila kinachotokea ni kwamba baadhi ya nchi zimeamua kuliangalia kwa mapana zaidi na baadhi wapo tayari kuendelea kuzuia uingizwaji wa hizo nguo.

Ninachotarajia mimi ni kwmaba huko tunakokwenda kila mtu ataweka utaratibu kuhakikisha kwamba tunaachana na matumizi ya nguo za mitamba lakini mimi nadhani si suala tu la biashara na viwanda pia kuna suala la utu pia.

Nchi ambazo zina biashara ya kuleta mitumba zinalalamika ni kwanini tuachane na kuvaa nguo ambazo wamevaa wao tayari. Jambo la msingi ni kwamba na wao wajue wakati umefika sasa tuangalie upya kama kweli ndivyo tunavyotakiwa kuwa. Ushirikiano wa kibiashara tunaotakiwa kuwa nao na hawa wenzetu kwa mazingira ya sasa inafaa wakaja wakaleta viwanda hapa hapa, wakatengeneza nguo ambazo ni mpya na tunazoweze kuzitumia.

Si kweli kwamba hatujui kwamba baadhi ya wananchi wetu hawana uwezo wa kifedha wa kuvaa baadhi ya nguo ambazo ni mpya lakini tunakoelekea tunaweza kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba tunaachana na hiyo hali ambayo tulikuwa anayo kwa muda mrefu.

Uamuzi mzito kama huo si wa hivi hivi, unakuja na gharama yake. Lazima watu wajiandae kukabiliana na dhahama ya uamuzi huo mkubwa lakini mimi nafikiri tuko vizuri katika hilo. Wale ambao wanaamini wapo tayari kuendelea waache waendelee na wale ambao wanataka kuliangalia hili suala upya lakini hawajaachana na wazo la kuachana na nguo za mitumba kwa lengo la kuinua viwanda vya ndani nao pia wajiwekee utaratibu wa kufanya hivyo. Huko tunakokwenda tutakutana tu, tutatakeleza kwa pamoja uamuzi ambao tulikubaliana.

SWALI: Unauzungumziaje uhusiano wa Rwanda na Tanzania ukizingatia kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeshafungua ofisi zake mjini Kigali?

JIBU: Uhusiano kwa ujumla ni mzuri sana na siku zote umekuwa mzuri. Hilo ni suala la ushirikiano baina ya nchi hizo mbili na mimi kama spika nabeba jumuiya. Lakini ni ukweli pia kwamba ushirikiano kijumuiya unategemea ushirikiano wa nchi mojamoja na jirani zake. Kwa hiyo ujirani mwema na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Rwanda na ambao umekuwepo siku zote ni muhimu sana katika ushirikiano wetu kama jumuiya.

Mfano ulioutoa wa uanzishaji wa ofisi za bandari Kigali nafikiri ni hatua nzuri sana ambayo imerahisisha utendaji kibishara.Hakuna ubishi kwamba biashara inategemea sana kasi ya utendaji, muda unaotumiwa kufanya miamala ya kibiashara moja hadi nyingine ni wa muhimu sana.

Juhudi zilizofanywa na TPA kupeleka ofisi zake Kigali zimesaidia sana kuokoa muda kwa upande wa wafanyabiashara wa Rwanda ambao walikuwa wanatumia muda mrefu kwenda Dar es Salaam kuondoa au kusafirisha mizigo yao toka bandari hiyo na kuisafirisha hadi Kigali.

Lakini pia napenda kupongeza juhudi zinazofanywa na serikali ya Tanzania kutekeleza miradi mikuwba ambayo kwa muda mrefu ilikuwa haijatekelezwa ingawa ni ya muhimu sana hasa kwa majirani wa zake. Hapa napenda kugusia mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambao serikali iliyopo sasa inautekeleza kwa haraka sana. Huu ni mradi mkubwa na ni wa muhimu sana kwa Tanzania lakini pia ni wa muhimu sana kwa majirani zake.

Lazima tuelewe kwamba nchi zilizobahatika kuwa na bandari zina jukumu la kijamii la kusaidia majirani ambao hawana nafasi hiyo. Katika kutekeleza hilo siyo suala la kuliangalia kibiashara tu bali ni vizuri pia likiangaliwa kiujirani mwema.

Hakuna ubishi, wengi hivi sasa tunafurahia namna ambavyo serikali ya sasa ya Mheshimiwa Rais John Magufuli inavyofanya kuhakikisha kwamba Ujenzi wa Reli ya Kisasa unapelekwa haraka ili iweze kufika kwa majirani zake Rwanda na Burundi. Hiyo itakuwa ni hatua kubwa sana ambayo itachochea kukua kwa uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashari na majirani zake.

Itaendelea Jumanne ijayo

Related Articles